1 Kings 17

Eliya Analishwa Na Kunguru

1 aBasi Eliya, Mtishbi kutoka Tishbi katika Gileadi, akamwambia Ahabu, “Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninamtumikia, hapatakuwa na umande wala mvua katika miaka hii, isipokuwa kwa neno langu.”

2Kisha neno la Bwana likamjia Eliya, kusema, 3 b“Ondoka hapa, elekea upande wa mashariki ukajifiche katika Kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yordani. 4 cUtakunywa maji kutoka kile kijito, nami nimeagiza kunguru wakulishe huko.”

5Hivyo akafanya kile alichoambiwa na Bwana. Akaenda katika Kijito cha Kerithi, mashariki ya Yordani na akakaa huko. 6 dKunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi na mkate na nyama jioni, naye akanywa maji kutoka kile kijito.

Mjane Wa Sarepta

7Baada ya muda, kile kijito kikakauka kwa sababu mvua haikuwa imenyesha katika nchi. 8Kisha neno la Bwana likamjia, kusema, 9 e“Ondoka, uende Sarepta ya Sidoni na ukae huko. Nimemwagiza mjane katika sehemu ile akupatie chakula.” 10 fHivyo akaenda Sarepta. Alipofika kwenye lango la mji, mjane alikuwa huko akiokota kuni. Akamwita na kumwambia, “Naomba uniletee maji kidogo kwenye gudulia ili niweze kunywa.” 11Alipokuwa anakwenda kumletea, akamwita akasema, “Tafadhali niletee pia kipande cha mkate.”

12 gAkamjibu, “Hakika kama Bwana Mungu wako aishivyo, sina mkate wowote, isipokuwa konzi ya unga kwenye gudulia na mafuta kidogo kwenye chupa. Ninakusanya kuni chache nipeleke nyumbani na nikapike chakula kwa ajili yangu na mwanangu, ili kwamba tule, kiishe, tukafe.”

13Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda nyumbani ukafanye kama ulivyosema. Lakini kwanza unitengenezee mimi mkate mdogo kutoka vile ulivyo navyo kisha uniletee na ndipo utayarishe chochote kwa ajili yako na mwanao. 14Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Lile gudulia la unga halitakwisha wala ile chupa ya mafuta haitakauka hadi siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.’ ”

15Akaondoka na kufanya kama Eliya alivyomwambia. Kwa hiyo kukawa na chakula kila siku kwa ajili ya Eliya, yule mwanamke na jamaa yake. 16Kwa kuwa lile gudulia la unga halikwisha na ile chupa ya mafuta haikukauka, sawasawa na lile neno la Bwana alilosema Eliya.

17Baada ya muda, mwana wa yule mwanamke mwenye nyumba akaugua. Hali yake ikaendelea kuwa mbaya sana, na hatimaye akaacha kupumua. 18 hAkamwambia Eliya, “Una nini dhidi yangu, ewe mtu wa Mungu? Umekuja ili kukumbushia dhambi yangu na kusababisha kifo cha mwanangu?”

19Eliya akamjibu, “Nipe mwanao.” Eliya akampokea kutoka kifuani mwake, akambeba mpaka chumba cha juu alipokuwa anaishi, akamlaza kitandani mwake. 20 iKisha akamlilia Bwana, akasema “Ee Bwana Mungu wangu, je, pia umeleta msiba juu ya mjane huyu ninayeishi pamoja naye, kwa kusababisha mwanawe kufa?” 21 jKisha akajinyoosha juu ya kijana mara tatu na kumlilia Bwana, akisema, “Ee Bwana Mungu wangu, nakuomba roho ya huyu kijana imrudie!”

22 Bwana akasikia kilio cha Eliya, na roho ya kijana ikamrudia, naye akafufuka. 23 kEliya akamtwaa kijana na kumbeba kutoka chumbani mwake akamshusha kumpeleka kwenye nyumba. Akampa mama yake na kusema, “Tazama, mwanao yu hai!”

24 lNdipo yule mwanamke akamwambia Eliya, “Sasa ninajua kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la Bwana kutoka kinywani mwako ni kweli.”

Copyright information for SwhNEN